We understand better that enim ad minim veniam, consectetur adipis cing elit, sed do

Tunapozungumzia Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Usharika wa Msasani, tunazungumzia wimbi la umisheni la kilutheri lililoanzia miaka ya 1850 mwanzoni ambapo wamisheni walutheri walikuja eneo la Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP). Walifika kulala Msasani tarehe 12-13/02/1850 (Kitabu cha J.L. Krapfs Reisen in Ostafrika) kabla ya kwenda eneo ambalo likawa ni kituo cha kimisheni maeneo ya Feri-Kivukoni. Hivyo eneo la Msasani ni miongoni mwa maeneo mwanzoni kukanyagwa na wamisheni ingawa kanisa katika ardhi ya Msasani lilikuja kujegwa miaka mingi sana baadaye.

 

Kama ambavyo jua linapoanza kuchomoza alfajiri ndivyo giza huanza kutoweka taratibu kwa kadiri muda unavyosogea; ndivyo ilivyokuwa kwa Usharika wa KKKT Msasani. Haukuibuka tu kama uyoga bali kuna mwanzo ambao kwa haraka usingeweza kufikiri kwamba utakuja kuwa sehemu ya kanisa ambalo Mungu ataruhusu litoe nuru kwa jamii kubwa ndani ya mkoa, Dayosisi na Nchi nzima kwa ujumla wake.

 

Kukua na kuongezeka watu Dar es salaam kulienda sambamba na umisheni kuenea katika Dayosisi ya Mashariki na Pwani na injili iliingia rasmi Dayosisi ya Mashariki na Pwani 1887 kuanzia Kisarawe na kusambaa kwingine kwingi. Pamoja na kwamba wamishenari wa Kilutheri waliingilia Pwani ya Dar es salaam (kutoka Zanzibar) lakini kazi yao ya kusambaza injili waliamua kuianzia nje ya Dar es salaam ambapo kwa sasa kunaitwa Mkoa wa Pwani. Kwa miaka hii ya mwanzoni ilikuwa kama kijiti kidogo ambacho kimewashwa moto na kuwekwa kwenye kuni mbichi, ila ajabu kwa neema ya Mungu moto wake haukuzimika na nuru yake haikuzuiliwa na giza.

 

Usharika wa Msasani ni matokeo ya wafanyakazi wa Kiafrika ambao walikuwa wafanyakazi wa nyumbani mwa wazungu na kazi zingine na wakiishi karibu na maeneo ya Msasani, Oysterbay, Makangira n.k mwanzoni mwa miaka 1950. Watu hawa walikuwa wanapata shida ya mahali pa kuabudia, kwani pamoja na kwamba maeneo machache Dar es salaam yalikuwa na makanisa ila yalikuwa mbali na eneo walilopo. Makanisa kama Magogoni, Azania Front, KKKT Usharika wa Kariakoo na KKKT Usharika wa Temeke yalikuwa tayari yameshaanza na wanayo maeneo ya kufanyia ibada. Wafanyakazi hao ambao walikuwa ni mchanganyiko kutoka makanisa ya Kilutheri, Anglikana, Moravian na African Inland Church wakawa ndio chachu kubwa ya kuanzishwa kwa Usharika wa KKKT Msasani. Pamoja na kwamba kuna mchango mkubwa sana kutoka kwa wamishenari Walutheri wazungu, bado pia Usharika wa KKKT Msasani ulitiwa chachu mno na wazalendo. Mfano mzuri ni Mwinjilisti ambaye baadaye alikuja kuwa Mchungaji ndugu Daudi Said Bundi. Yeye alikuwa akienda kufanya ibada katika Gereza la Oysterbay ambako wafungwa walihubiriwa habari njema ya ufalme wa Mungu. Mwanzo wa Usharika wa KKKT Msasani haukuwa mwanzo unaovutia ila ni mwanzo unaosisimua na kuonesha namna nuru inapoanza kuingia gizani basi giza halina budi kuipisha nuru hiyo.

 

Wafanyakazi hao ambao hawakuwa na eneo maalumu la kufanyia ibada waliamua kuwa wanakusanyika chini ya mti wa mbuyu na kumfanyia Mungu ibada. Kwa kusaidiwa na mkristo mmoja aliyekuwa afisa magereza waliweza kuanza kufanyia ibada ndani ya magofu hayo ya magereza. Eneo hilo kwa sasa ndipo zilipo ofisi za Usalama wa Taifa Osysterbay. Kuabudia katika magofu hayo ilikuwa ni ahueni kulinganisha na chini ya mbuyu, lakini baada ya muda fulani, serikali ilihitaji kuendeleza maeneo hayo. Hivyo washarika hawa wakawa na changamoto ile ile ya awali ya eneo la kufanyia ibada. Wakaendelea kufanyia ibada chini ya mbuyu, Mungu aliwasaidia wakapata eneo lingine Kinondoni sehemu ya Mtambani. Hamahama ya eneo la kuabudia kwa ndugu hawa siyo kwamba lilifumbiwa macho na viongozi wa juu kwani ofisi ya Sinodi iliwajengea kanisa la kwanza la Magomeni Mviringo. Maeneo yote ambayo watu hawa walipita waliacha nuru inang’aa na maeneo hayo hadi leo kuna maendeleo ya kijamii. Hii ni ishara tosha kwamba eneo lolote amabalo kanisa lilipita liliacha uhai na uhai huo umedumu hata leo. Hivyo yale maneno aliyoyasema Yesu “Ninyi ni nuru ya ulimwengu,” “Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu yam lima.” – Mathayo 5:14 yanaonekana Dhahiri. Inazidi kuonekana hata leo kwamba palipo na kanisa basi nuru itaangaza tu.

 

Watumishi waliowahi Kutumika Usharikani

 
#majinamiaka ya uongozi 
1Mchg. Lloyd SwantzTangu Oysterbay mpaka miakaya 1960 na 1963Mwamerika( USA)
2Mchg. Ronald T. Englund1964-1966Mwamerika( USA)
3Mchg. M.K. Jahnel1966-1970Mjerumani(GERMAN)
4Mchg. Samwel Dimwaya1976 – 1981Marehemu
5Mchg. Dkt Gabriel Nzalayaimisi1981-1984Yuko SUA, Jordan University College, St. Augustine of Tanzania, Director – Kana Secondary School
6Mchg. Msafiri Chagulilo1984-1985Marehemu
7Mchg. Heriel Mwakabonga1985-1986Mstahafu
8Mchg. Charles Chuma1986-1991Mkuu wa Jimbo- Marehemu
9Dean Adam Kombo1991-1999Amekuwa Msaidizi wa Askofu – Marehemu
10Mchg. Abraham King’omela1999-2000Amekuwa Mkuu wa Jimbo – Mstaafu – Marehemu
11Mchg. Abraham Kilindo2000 – 2001Mstahafu
12Mchg. Daniel Mbowe2001 – 2002Mchungaji Kiongozi Ush. Kipawa
13Askofu Dkt Alex Gehaz Malasusa2002 – 2003Askofu KKKT DMP na Askofu Mkuu wa KKKT aiiyemaliza muda wake
14Mchg. Dkt Enock Mlyuka2003-2005Naibu Katibu Mkuu – DMP
15Mchg. Lewis Hiza2005-2008Chaplain DSM University
16Askofu Chediel Elinaza Sendoro2008 – 2011Askofu KKKT Dayosisi ya Mwanga
17Mchg. James Ngalla2011 -2012Mchungaji wa Usharika wa Yombo Dovya
18Mchg. Eliguard Metili2012 – 2018Mchungaji Kiongozi Usharika wa Kinyerezi
19Mchg. Manford Kijalo2018 mpaka sasaMchungaji Kiongozi Usharika wa Msasani
20Mchg. Manase Lema2016 – 2019Mchungaji Usharika wa Msasani
21Mchg. Margret Shekolowa2019-mpaka sasaMchungaji Usharika wa Msasani
 

Wasemavyo Kuhusu Usharika wa Msasani

Nimemuona Mungu katika mwanzo mdogo wa Usharika huu wa Msasani. Tangu kipindi ambacho tulikuwa tunafanya ibada chini ya mti, pale ambapo kwa sasa limejengwa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Petro (St. Peter). Tulikuwa watu wa kawaida sana, wenye uwezo mdogo; watu wengi wenye uwezo mkubwa wa maeneo ya Msasani na Oysterbay walikuwa wakienda kuabudu katika Usharika wa Azania Front. Nimeshuhudia Kanisa likijengwa na likikua hatua kwa hatua, hakika Mungu huwatoa watu mavumbini na kuwaketisha na wakuu. Haya yanayoonekana leo ni matokeo ya mwanzo mdogo pamoja na Mungu, yule tuliyemwamini na kumwabudu hata wakati tungali chini ya mti; ndiye huyo huyo ametufanya kuwa moja ya Sharika za Baraka katika Dayosisi yetu ya Mashariki na Pwani”.
Askofu Dkt. Peter Mwamasika Mwinjilisti Usharika wa Msasani miaka ya 1955 – 1964.

 

“Nimekuwa msharika wa Usharika wa Msasani toka mwaka 1964 nikiwa mtoto wa Shule ya Jumapili (Sunday School), nilipata ubarikio katika Usharika huu huu. Kanisa hili lilijengwa kwa ajili ya wafanyakazi wa ndani ambao walikuwa wakifanya kazi za ndani na kuzunguka nyumba, lakini pia kwa ajili ya familia chache sana ambazo walikuwa wakifanya kazi serikalini na katika mashirika ya umma. Wafanyakazi wengi wa serikali na wafanyabiashara walikuwa wakienda kuabudu katika Usharika wa Azania Front Posta. Kwa muda wote huu nimeshuhudia Mungu akitusaidia kupiga hatua kwa hatua katika maendeleo kuanzia tukiwa na wachungaji wageni hadi wazawa, kanisa kutoka kuwa tegemezi hadi kufika hatua ya kutegemeza wengine, kutoka washarika wachache na kuwa washarika wengi, kutoka kuwa na miradi midogo hadi kuwa na miradi mikubwa. Hayo yote yanadhihirisha bila chenga kwamba kazi ya Mungu wa kweli na Neno lake vitadumu milele na yupo pamoja nasi hadi ukamilifu wa dahari.”
Mchungaji Lewis Hiza Mchungaji Kiongozi Usharika wa Msasani 2007 – 2009