Wimbo huu ulitungwa na Priscilla Jane Owens (1829–1907); Alikuwa mwalimu wa shule ya Jumapili, mwandishi wa nyimbo, na mfanyakazi mmisionari kutoka Baltimore, Maryland – Marekani. Priscilla anajulikana kwa nyimbo zake zilizoandikwa kwa ajili ya watoto na vijana, hasa inayolenga mikusanyiko ya wamishonari na Uinjilisti. Nyimbo zake zilibeba jumbe dhabiti za imani, ujasiri, na uinjilisti, zikiambatana na harakati za umisionari katika karne ya 19. Moja ya nyimbo zake maarufu ni huu unaoitwa “Tumesikia Mbiu”, ambao huimbwa sana makanisani na katika mikutano ya injili.
Wimbo huu ni wito wenye nguvu wa kueneza ujumbe wa wokovu kote ulimwenguni. Tumeisikia Mbiu ulichapishwa kwa mara ya kwanza katika Jarida la Machapisho ya Nyimbo na Tenzi la mwaka 1882 lililojulikana kama “1882 Hymnals Glad Hallelujaha.” Sauti za wimbo zilitungwa na John R. Sweney akishirikiana na John Kirkpatrick. Wimbo huu ulipata umaarufu wakati wa mikutano ya uamsho, haswa kwa sababu ya sauti yake ya nguvu na ya kurudia “Yesu Loo! Aponya! Yesu Loo! Aponya!”
Sauti inayosisitiza kueneza ujumbe wa injili kwa mataifa yote; ujumbe ambao ulikuwa msingi wa harakati ya umisionari ya karne ya 19. Priscilla alishawishiwa na Utume Mkuu kwenye Mathayo 28:19-20, unaotuita Wakristo kueneza injili kwa mataifa yote. Mama huyu aliamini sana katika ufikiaji (outreach) wa Kikristo na Misioni na alitaka kuunda wimbo ambao ungewahimiza waumini kushiriki ujumbe wa wokovu kupitia Yesu Kristo.
Hakika Tumeisikia Mbiu, Yesu Loo Aponya. Tuimbe wimbo huu na kuineza injili kwa wote.