Wimbo huu ni moja ya nyimbo maarufu sana za Pasaka. Uliandikwa mwaka 1874 na Robert Lowry, Mchungaji wa Kibaptisti kutoka Marekani. Wimbo unasherehekea ufufuko wa Yesu Kristo, ukilinganisha huzuni ya kaburi na ushindi wa kufufuka Kwake kwa furaha kuu. Katika uimbaji wake, wimbo unaanza polepole na kwa huzuni, lakini kiitikio chake hupasuka kwa shangwe na ushindi.
Ulichapishwa kwa mara ya kwanza katika kitabu cha nyimbo “Brightest and Best,” kilichohaririwa na Lowry pamoja na W. H. Doane. MLE KABURINI, YESU MWOKOZI ulipata umaarufu haraka katika makanisa ya Kiprotestanti ya Marekani na hivi sasa umeendelea kuwa sehemu ya ibada za Pasaka kote ulimwenguni.
Mch. Lowry aliandika maneno na pia akatunga muziki wa wimbo huu, jambo lisilo la kawaida kwa tenzi nyingi za karne ya 19 kwa mujibu wa kumbukumbu za vitabu vya nyimbo. Mch. Lowry alipenda sana muziki na aliandika zaidi ya nyimbo 500, ikiwa ni pamoja na tenzi maarufu kama “Shall We Gather at the River?”, “Christ Arose (Low in the Grave He Lay)”, na “Nothing But the Blood of Jesus.”
Tunapoendelea kushangilia ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, karibuni sote tuimbe “Bwana Amefufuka, kifo kimeshindwa kabisa; Yu hai, Yu hai, Yesu Mwokozi”
